What's New
Speeches
Mkereketwa
Official Policy Documents
Official Working Documents


KUMBUKUMBU KUMUENZI BABA WA TAIFA

Tarehe 14 Oktoba, 2009, Taifa letu linaadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kumi baada ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere. Katika kufanya hivyo, inafaa pia tujikumbushe mambo ya msingi ambayo Baba wa Taifa aliyapa kipaumbele cha juu kabisa wakati wa uongozi wake. Madhumuhi ya makala hii ni kukumbusha baadhi ya mambo hayo.

 

Jambo la kwanza lilikuwa ni kujenga taifa lenye umoja na mshikamano

 

Baba wa Taifa mwenyewe alithibitisha umuhimu mkubwa aliouweka katika kujenga Taifa lenye umoja, katika hotuba yake aliyoitoa Bungeni tarehe 29 Julai, 1985, wakati akiliaga rasmi Bunge kabla ya kustaafu kazi ya urais wa Tanzania.  Baba wa Taifa alisema hivi:-

 

 ‘‘Kazi iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi, niliyoiazimia katika hotuba yangu ya kwanza Bungeni mwezi Desemba 1962, ilikuwa ni kazi ya kujenga Taifa lenye umoja kwa msingi wa heshima na usawa wa binadamu. Aidha, nilipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka mmoja kabla ya hapo, vile vile nilitoa ahadi kwamba msingi wa vitendo vya Taifa letu utakuwa ni kufanya  jitihada za dhati za kudumisha  heshima na usawa wa binadamu nchini mwetu, na mahali pengine duniani. Nadhani naweza nikasema bila kusita, kwamba mnamo chini ya miaka 25 ya uongozi wangu, kwa upande wa shabaha hii kuu na ya msingi kupita zote, tunayo haki ya kujivuna. Sasa tunalo taifa lenye umoja, na taifa ambalo msingi wake ni heshima na usawa wa binadamu.’’

 

 

 

 

Inafurahisha kuona kwamba Mwalimu Nyerere mwenyewe aliridhishwa na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake kuhusu masuala hayo muhimu.  Kwa hiyo katika kumkumbuka na kumuenzi, hatuna budi kuendelea kuyatekeleza.

 

Taifa linaloheshimu usawa wa binadamu

 

Ni muhimu kutambua kwamba kuna vipengele viwili ambavyo vinapaswa kuzingatiwa katika maneno hayo ya Baba wa Taifa, ambavyo ni:-

 

(a)            Kudumisha Umoja wa Taifa;

(b)            Kudumisha misingi ya heshima kwa kila mtu na usawa  wa binadamu.

Kuhusu kipengele cha kujenga umoja wa taifa letu, hatuna budi kumkumbuka na kumuenzi kwa hatua mahsusi alizozichukua za kutekeleza azma yake hiyo ya kujenga umoja wa taifa letu. Miongoni mwa hatua hizo  ni ile ya kutaifisha shule zote za madhehebu ya dini zilizokuwapo wakati huo, ambazo zilikuwa zinasomesha wafuasi wa dini zao tu; na kuzifanya ziwe shule za serikali ili ziweze kusomesha mwanafunzi yeyote yule, bila ubaguzi wa  kidini. Baba  wa Taifa alifanya hivyo kutokana na kubaini hatari iliyokuwapo katika mfumo huo wa elimu uliokuwa wa kibaguzi kwa misingi ya dini. Hatari yenyewe  ilikuwa ni kwamba kwa kuwa Waislamu hawakuwa na shule za aina hiyo, na kwa kuwa shule za Serikali zilikuwa ni chache mno, matokeo yake yangekuwa ni kwamba watu wengi zaidi ambao wangepata elimu wangekuwa ni wa madhehebu ya kikristo tu, na ndio peke yao wangejipatia sifa za kuwa na elimu inayotosha kuajiriwa katika utumishi wa serikali na kwingineko. Hali hiyo ya ubaguzi wa kidini ingewaacha waislamu nje kabisa ya shughuli za uendeshaji na utawala wa nchi.

 

Ni dhahiri kuwa hali hiyo ingekuwa ni kikwazo kikubwa katika ujenzi wa taifa lenye umoja. Ndiyo sababu alichukua hatua za haraka kuzitaifisha shule zote hizo. Tunao wajibu wa kumkumbuka na kumuenzi kwa kitendo chake hicho.

 

Chimbuko la Azimio la Arusha

 

Aidha, tukitafakari vizuri, tutagundua kuwa ule msingi wa ‘heshima kwa kila mtu na usawa wa binadamu’ ndio baadaye  uliozaa Azimio la  mwaka 1967, kuhusu siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kwa hiyo katika kumuenzi Baba wa Taifa kwenye jambo hilo, hatuna budi  kurejea kwenye Azimio la Arusha, pamoja na kujikumbusha jinsi Azimio la Arusha lilivyopata misukosuko mingi mwanzoni mwa miaka ya Tisini.  Misukosuko ambayo ilitokana na uamuzi  wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Februari 1991, unaoitwa ‘Azimio la Zanzibar’ linalodaiwa kwamba ‘liliua’ Azimio la Arusha.

 

Kwa hiyo nashauri kwamba katika kumuenzi Baba wa Taifa kwa upande wa Azimio la Arusha, inafaa kwanza tukubali kwamba ingawa yapo baadhi ya  mambo ndani ya Azimio la Arusha ambayo tunaweza bado kuyaendeleza, lakini vile vile tukubali  kwamba katika dunia ya leo, yapo mambo mengine ndani yake ambayo hatuwezi kabisa kuyarejesha.

 

        Ili tuweze kubaini vizuri ni mambo gani tunaweza kuyaendeleza, na yapi hatuwezi kuyarejesha, ni muhimu tujikumbushe tena maudhui ya Azimio hilo.

 

Ni vizuri kufanya hivyo kwa sababu Baba wa Taifa aliwekeza nguvu kubwa pamoja na akili zake nyingi katika kuliandika, kulielezea au kulitolea ufafanuzi, na kwa kulitetea Azimio la Arusha. Kwa hiyo katika kumkumbuka na kumuenzi, yafaa tujikumbushe maudhui yake.

 

 

 

Maudhui ya Azimio la Arusha

Katika sehemu yake ya kwanza  Azimio la Arusha kwanza linataja madhumuni na shabaha zake. Awali Mwalimu Nyerere alielezea chanzo cha Azimio la Arusha, katika hotuba yake ya tarehe 10 Desemba, 1962, wakati akifungua Bunge jipya la  Jamhuri ya Tanganyika. Alisema hivi:

 

“Neno linalofaa kuelezea nia na  madhumuni ya serikali yetu, ni ‘ujima’. Kwani ujima ni mfumo wa kuishi na kufanya kazi kidugu.”

 

Baadaye, katika Andiko lake lililopewa kichwa cha habari cha ‘Shabaha ni Binadamu’, Baba wa Taifa aliainisha kwamba kwa upande wa uchumi, lengo kuu la Azimio la Arusha lilikuwa ni kuinua ubora wa maisha ya Watanzania wote katika ujumla wao, kwa kutumia mbinu zifuatazo:-

 

(a)            Kuondoa unyonyaji wa mtu mmoja kumnyonya mwingine. Mkakati ukiwa ni kuhakikisha kwamba kila  mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, anafanya  kazi, kwa kuwawezesha wakulima kuishi pamoja katika vijiji vya ujamaa, na kufanya kazi kwa pamoja kwa faida ya wote.

 

(b)            Kwa Dola kumiliki njia kuu zote za uchumi wa nchi.

 

(c)             Kwa kuhakikisha kuwa kuna demokrasia katika kuendesha utawala wa nchi.

 

Katika sehemu yake ya pili, Azimio la Arusha pia linazungumzia suala kubwa la kujitegemea, katika juhudi za kulitoa taifa letu kutoka katika hali ya dhiki,  na kuliweka katika hali ya neema. Ni vizuri ikumbukwe kwamba  kichwa chake cha habari kwa ukamilifu wake ni “Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Ujamaa na Kujitegemea” Kwa hiyo suala la kujitegemea limechukua sehemu kubwa sana katika Azimio hilo.

 

Katika sehemu yake ya tatu, Azimio la Arusha linazungumzia umuhimu wa kuwa na Viongozi bora, kwa hiyo linaweka miiko ya uongozi; ambayo inasema kwamba kiongozi wa chama chetu sharti:

 

(a)            Awe ni mkulima au mfanyakazi, na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au kikabaila.

(b)            Asiwe na hisa katika makampuni yoyote.

(c)             Asiwe Mkurugenzi katika Kampuni ya kibepari au kikabaila

(d)            Asiwe na mishahara miwili au zaidi.

(e)            Asiwe na nyumba ya kupangisha.

 

Katika sehemu yake ya nne, Azimio la Arusha linazungumzia umuhimu wa kuwa na wanachama bora, kwa kuweka mkazo kwenye suala la mafunzo ya itikadi kwa kila mwanachama. Azimio linasema kwamba ni lazima “wanachama wafundishwe kwa ukamilifu imani ya Chama chetu ili waielewe, na wakumbushwe wakati wote umuhimu wa kuishi kwa kuzingatia imani hiyo.”

 

Mambo ya Azimio la Arusha ambayo yanawezekana kuendelezwa, na  yale yasiyowezekana kurejeshwa

 

Tukifanya uchambuzi wa kina zaidi wa Azimio la Arusha, tutaona kwamba kwa kuwa chanzo chake ni “ujima”, yaani mfumo wa kuishi pamoja kama ndugu, tutatambua kwamba mfumo huo wa maisha unaweza bado kuendelezwa. Tutatambua vile vile kwamba suala la kujitegemea katika kufanikisha maendeleo yetu, bado linaweza kuendelezwa. Lakini  inafaa tukubali pia kwamba yapo mambo mengine ambayo haiwezekani tena kuyarejea.

 

Mambo ya Azimio hilo ambayo hayawezekani tena kuyarejea

Jambo moja katika Azimio la Arusha ambalo  ni dhahiri kabisa kwamba hatuwezi kulirejesha, ni lile suala la kutaifisha  njia kuu za uchumi na kuziweka chini ya umiliki wa Dola. Ni vema tukumbuke kwamba hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya Tisini, yalikuwa yametokea mabadiliko mengi na makubwa sana ya kiuchumi duniani kote tangu Azimio la Arusha  lilipotangazwa mwaka 1967. Mabadiliko hayo pia yaliathiri maisha ya watanzania kwa kiasi kikubwa sana.

 

Athari kubwa  zaidi kwa watanzania ilisababishwa na uhaba  mkubwa wa bidhaa, kutokana na uzalishaji mdogo wa bidhaa hizo  kutoka katika viwanda vyetu vya umma vilivyokuwapo. Wananchi walikumbwa na tatizo la kuwapo kwa uhaba mkubwa wa bidhaa wanazozihitaji katika maisha yao ya kila siku,  hali iliyosababisha kuwapo kwa  misururu mirefu ya watu kwenye maduka, ya Umma ya RTC yaliyokuwapo.

 

Kwa hiyo ili kukabilisha na hali hiyo ya dhiki kwa wananchi, Chama chetu kiliamua  rasmi kubadilisha sera zake za kiuchumi, kwa kuruhusu  sekta binafsi  iweze kushiriki katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani, ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wananchi. Hakuna kurudi nyuma katika suala hilo.

 

Tuzingatie Mwelekeo mpya wa sera za Chama za kiuchumi

        Ni vizuri tujikumbushe vile vile kwamba yalikuwa yametokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi Duniani kote tangu Azimio la Arusha lilipotangazwa mwaka 1967, mabadiliko ambayo pia yaliathiri maisha ya Watanzania.  Ndiyo sababu mwanzoni mwa miaka ya Tisini CCM iliamua rasmi kuhuisha sera zake kiuchumi kwa kutangaza mwelekeo mpya wa sera hizo kama ifuatavyo:-

 

        “Lengo la Ujamaa na Kujitegemea katika miaka ya Tisini litakuwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu, ama mwananchi mmoja mmoja, ama kwa kupitia vyama vyao huru vya ushirika, au kupitia makampuni ambamo wananchi watanunua hisa.  Kwa mpango huu, sehemu kubwa ya uchumi wa nchi itamilikiwa na wananchi wenyewe, na hii itawawezesha kuinua hali ya maisha yao, na kutosheleza mahitaji yao ya msingi.”

 

        Kwa hiyo mojawapo ya malengo ya maamuzi ya Zanzibar ilikuwa ni kuwawezesha wana-CCM kushiriki kikamilifu na kuendesha uchumi wa nchi, kulingana na mwelekeo huo mpya wa sera za uchumi za CCM kwa kuwawezesha kununua hisa katika makampuni ambayo yangeingizwa katika soko la hisa.

 

Azimio la Arusha na Miiko ya Uongozi

Katika hotuba yake kwenye klabu ya waandishi wa Habari ya tarehe  13 Machi, 1995, mjini Dar es Salaam, Mwalimu Nyerere alisema hivi kuhusu tatizo la kutokuwapo kwa miiko ya uongozi wakati huo:

 

‘Azimio la Arusha lilikuwa na miiko ya uongozi. Hakuna serikali popote duniani inayoendeshwa bila miiko. Waingereza wana miiko, Marekani wana miiko, Wafaransa wana miiko. Wajapani wana miiko. Huwezi kuendesha nchi hivi hivi tu bila miiko. Nchi zote zina miiko. Hapa kwetu sasa hatuna. Wameacha miiko ya Azimio la Arusha. Hawakuweka miiko mingine.’

 

Bila shaka Mwalimu Nyerere alikuwa akiwasemea watanzania wengi waliokerwa na lile Azimio la Zanzibar linalosadikiwa kuwa ‘liliua’ Azimio la Arusha hususan miiko ya uongozi iliyokuwamo. Bahati njema, maneno hayo ya Mwalimu Nyerere yalizingatiwa ipasavyo na serikali, kwani baadaye mwaka huo huo, serikali iliwasilisha Bungeni muswada wa sheria ulioweka masharti mapya ya viongozi wote wa Umma, pamoja na kuunda  Sekretarieti ya kusimamia maadili ya viongozi hao.

 

Sheria hiyo inatamka wazi kwamba kiongozi yeyote atakayeshindwa kutekeleza masharti yaliyomo humo, moja kwa moja atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye uongozi alio nao. Hakuna haja ya kumtaka kiongozi huyo ajiuzulu, au afukuzwe.

 

Kwa hiyo katika kumuenzi Baba wa Taifa kwa juhudi zake za kusimamia maadili na miiko ya viongozi, yafaa tutambue kwamba hivi sasa tatizo siyo tena kutokuwapo kwa Miiko ya uongozi. Miiko hiyo tunayo, tena imeandikwa  ndani ya sheria husika. Tatizo lililopo sasa ni kukosekana kwa usimamizi makini wa kuhakikisha kwamba miiko hiyo inatekelezwa vizuri na kila kiongozi anayehusika, na kwamba asiyetekeleza wajibu wake anaadhibiwa ipasavyo.

 

 Methali ya Mwalimu Nyerere ya ‘mficha ficha  maradhi’

Baba wa Taifa alikuwa mara kwa mara akitumia methali isemayo kuwa ‘mficha ficha maradhi, kilio humfichua.’ Katika utaratibu huu wa kumkumbuka na kumuenzi, Hatuna budi kukiri upungufu huo tulio nao  wa kutokuweka usimamizi makini wa maadili  ya viongozi wetu. Endapo tulificha upungufu huo, sasa kilio dhidi ya vitendo viovu vya baadhi ya viongozi wetu, vitendo ambavyo vimepewa jina la ufisadi, sasa kimetuumbua. Kwa hiyo ni lazima tuchukue hatua za kujisahihisha, kwa maana ya  kwamba ni lazima viongozi watakaobainika kuvunja miiko ya uongozi au kujihusisha na vitendo vya ufisadi, wachukuliwe hatua mara moja na Kamati zetu za Maadili.

 

Methali ya Mwalimu Nyerere ya ‘Mtoto akichezea wembe’

 

        Lengo hilo la kuwachukulia hatua mara moja  viongozi wanaokiuka  maadili  mema, pia linatukumbusha mafundisho mengine ya Baba wa Taifa,  aliyokuwa  akiyatoa  kwa  kutumia  methali  ya “ mtoto akichezea wembe, utamkata pale pale. Hausubiri mpaka baadaye”.  Matumizi yake ya methali hiyo kwa kweli yalikuwa ni maelekezo rasmi kwa vikao vyenye mamlaka ya kuwachukulia hatua, vifanye hivyo mara moja, au bila kuchelewa; kwama ambavyo wembe unavyomkata mara moja mtoto anayeuchezea.

 

 Umuhimu wa Kusimamia Maadili ya Viongozi

Kwa hiyo katika kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo, hatuna budi kujituma kusimamia maadili ya Viongozi kwa nguvu mpya. Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi, katika kikao chake cha Butiama cha mwezi Machi, 2008, kiliazimia kama ifuatavyo:-

 

‘Halmashauri Kuu ya Taifa imesikitishwa na ukiukwaji wa maadili na miiko ya uongozi ambao umejidhihirisha, hususan miongoni mwa viongozi walioko Serikalini.  Halmashauri Kuu ya Taifa imeazimia kuondoa upungufu huu, kwa kuelekeza yafuatayo:-

 

(a)            CCM haina budi kujiimarisha katika taswira yake ya asili kama Chama chenye viongozi waadilifu, na Chama kinachojali maslahi ya watu

 

(b)           Kwa ajili hiyo, Viongozi watakaobainika kuvunja miiko ya uongozi lazima  wachukuliwe hatua mara moja na  Kamati za Maadili za ngazi zote  ambazo lazima sasa zitekeleze majukumu yake ipasavyo, na kwa nguvu mpya.’

 

 Hatua hiyo ndiyo itaturejesha kwenye utekelezaji wa maelekezo ya Baba wa Taifa kupitia methali yake ya “mtoto akichezea wembe, utamkata pale pale”. Kwa hiyo katika kumkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa, hatuna budi kuhakikisha kuwa maazimio haya ya Butiama yanayohusu maadili ya viongozi wetu, yanatekelezwa kwa vitendo halisi vinavyoonekana dhahiri machoni kwa wanachama wetu.

 

 

 

 

Azimio la Arusha na mafunzo ya Itikadi:

 

Kutokana na Azimio la Arusha kupata misukosuko mingi kama nilivyoeleza mapema, suala la mafunzo ya itikadi kwa wanachama na viongozi wake liliachwa kabisa. Vyuo vilivyokuwa vya Chama chetu vya Kivukoni na vile vya Kanda, vilifungwa na kukabidhiwa Serikalini. Aidha Mafunzo ya miezi mitatu yaliyokuwa yakitolewa kwa waombaji  wapya wa uwanachama wa CCM, pia yalisitishwa. Matokeo yake yakawa ni wanachama kukosa msimamo.

 

Hadithi ya Mwalimu Nyerere ya “mtoto wa jongoo”

 

Kuhusu mafunzo ya itikadi kwa viongozi na wanachama wa CCM, Mwalimu Nyerere alipenda mara kwa mara kutumia hadithi ya mtoto wa jongoo, ambaye mara baada ya kuzaliwa na kujikuta ana miguu  mingi, alimuuliza mama yake kwamba je mama, miguu yote hii nikitaka  kutembea nianze na mguu upi? Mama yake akamjibu: ‘wewe tembea tu, miguu itajua yenyewe jinsi ya kujipanga’.  Kwa  kitendo kile cha kufuta mafunzo ya  wanachama, na sisi  kwa kweli tulijiweka katika hali ya kutoa majibu kama hayo ya mama jongoo. Kwani tunapowachagua viongozi wetu na kuwaacha bila kuwapa mafunzo yoyote ya kuwasaidia katika uongozi wao, ni kama tunawaambia “wewe nenda tu, ‘utajua mwenyewe namna  ya kufanya kazi zako za uongozi”.

 

Kwa hiyo katika kumkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa kwa juhudi zake za kujenga Chama chenye itikadi na mwelekeo mzuri, hatuna budi kufufua kwa nguvu mpya suala hili la mafunzo ya itikadi na maadili kwa viongozi na wanachama wetu.  Ni bahati njema kwamba, miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa kule Butiama, lipo azimio la kufuufua utaratibu wa mafunzo ya itikadi na maadili kwa makada wa Chama chetu; pamoja na kuharakisha utekelezaji wa mpango wa uanzishwaji wa vyuo vipya vya mafunzo, ambao tayari umekwisha kuanza.  Hali kadhalika, kama sehemu ya jitihada za kupata viongozi waadilifu katika Chama chetu, Halmashauri Kuu ya Taifa katika mkutano wake huo  iliazimia vile vile kwamba uwekwe utaratibu bora zaidi wa kuwachuja wagombea wa nafasi za uongozi katika Chama, katika vyombo vya Dola, ili  tuweze kuwabaini mapema  na kuwaacha  wale  wote ambao hawana sifa ya uadilifu.

 

Mwalimu Nyerere na mapambano dhidi ya rushwa

Jambo lingine zito na la msingi ambalo Baba wa Taifa alilipatia kipaumbele kikubwa sana, ni mapambano dhidi ya rushwa. Katika  hotuba yake aliyoitoa Bungeni tarehe 17 Mei, 1960, alisema maneno yafuatayo kuhusu adui rushwa:

 

‘Nilikwisha kusema mahali pengine kwamba sera ya serikali  yetu mpya baada ya uhuru, itakuwa ni kupambana na maadui watatu, yaani umaskini, ujinga na maradhi. Lakini  leo napenda kuongeza adui mwingine kwenye orodha hiyo, naye ni adui rushwa. Tusipopambana vikali na rushwa, wananchi watakosa imani na serikali yao. Ni lazima tupigane na  adui rushwa kwa nguvu sawa na zile tunazozitumia katika kupingana na adui wakati wa vita. Nionavyo mimi ni kwamba wahalifu wa rushwa wanastahili kuadhibiwa  sawa na wahalifu wa uhaini.’

               

Katika hotuba yake nyingine ya tarehe  13 Machi, 1995, aliyoitoa Mbeya kwenye Sherehe za Mei Mosi, Baba wa Taifa alisema hivi:

 

‘Wala msije mkadhani kuwa wakati wa awamu yangu ya uongozi  palikuwa hapana rushwa. Ilikuwapo. Lakini tuliidhibiti kwa kuwa wakali sana. Tulipitisha sheria yenye masharti makali kwamba mtu akisha kuthibitika mahakamani kwamba katoa rushwa, atakwenda jela kwa muda usiopungua miaka miwili, pamoja na kuchapwa viboko ishirini na vine, kumi na viwili siku anayoingia, na kumi na viwili siku anayotoka.’

 

Kwa kuwa tumeazimia kumkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa, basi hatuna budi tuwe wakali kama alivyokuwa yeye katika


published:
14:01:21 18.09.2009

   

Habari Zaidi:

   
     

ccm flag



Email
Links
Contact Us
CCM Creed   Conditions for Membership   Aim and Objectives

Chama Cha Mapinduzi believes that all human beings are equal

 

It is easy to be a member of CCM as its conditions for membership are directed towards an integrity citizen

 

CCM aims at defending the independence of our country and the freedom of its citizens

© COPYRIGHT 2002-2010
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
P.O. BOX 50, DODOMA - TANZANIA [TELEFAX: +255-22-2185245; EMAIL: katibumkuu@ccmtz.org]